Saturday, November 9, 2013

MASHAUZI KUONGOZA UZINDULIZI WA MALAIKA HIVI KARIBUNI.

BENDI ya muziki wa taarabu ya Mshauzi Classic, Cassim Mganga na Dully Sykes, watasindikiza uzinduzi wa bendi mpya ya Malaika utakaofanyika Novemba 15, mwaka huu katika ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa bendi hiyo, Michael Rocky, alisema tayari walikubaliana na bendi na wasanii hao kushiriki katika uzinduzi wao.

"Tuliwaomba kama wasanii wenzetu, walikubali na kutuahidi kutoa burudani nzuri katika onesho hilo maalumu la kuzaliwa kwa bendi mpya," alisema.

Alisema wasanii hao, ni miongoni mwa wasanii wanaopendwa na mashabiki wa muziki kutokana na tungo zao kuwa na ujumbe mzuri.

Rocky ambaye aliwahi kuiongoza Akudo Impact kwa mafanikio, alisema watatumia uzoefu wao kuhakikisha bendi yao inaingia katika soko la muziki kwa nguvu.

Bendi hiyo mpya tayari imerekodi nyimbo mbili, moja ikiwa imetengenezwa kwenye video na kusambazwa katika vituo mbalimbali vya teklevisheni.

Rocky alizitaja nyimbo hizo ni Nakuhitaji.ambao umerekodiwa katika video na Mtu wa Watu, lakini tayari wameandaa nyimbo sita.

"Tuna nyimbo sita zilizofaniwa mazoezi, mbili zimerekodiwa, nne bado hazijarekodiwa, zote zitasikika siku ya uzinduzi wa bendi yetu," alisema Mkurugenzi huyo.

Bendi hiyo ya Malaika inaongozwa na Mfalme Christian Bella, Katibu Mkuu ni Andrew Sekedia akisaidiwa na Emmanuel Karonji 'Totoo Zebingwa.

TANZANIA TOP MODELS WAINGIA KAMBINI RASMI.


SHINDANO la Taifa la mitindo lijulikanalo kama Tanzania Top Models waingia kambini rasmi jana katika hoteli ya JB Belmont iliyopo katikati ya jiji Dar es Salaam.

Kambi hiyo iliyowajumuisha jumla ya wanamitindo 20 ilianza rasmi kwa waandaji wao kuwapa somo warembo hao jinsi ya kuishi kwa upendo katika kipindi chote watakachokuwa kambini.

Akizungumza na wanamitindo hao mwenyekiti wa kamati hiyo Jackson Kalimkumtima aliwaasa warembo hao kuishi kwa kushirikiana na upendo kwa muda wote watakaokuwa pamoja katika kambi hiyo.

Jackson aliongeza kuwa ndani ya kipindi chote cha warembo hao watakachokaa kambini wapenzi wa fani ya mitindo nchini watapata fursa ya kutazama maisha ya wanamitindo hao kupitia kituo cha televisheni cha Clouds.

Naye mkufunzi wa wanamitindo hao Zakia Twahili naye aliwasisitizia swala la heshima miongoni mwa warembo hao kwa muda wote watakaokuwa pamoja.

Shindano hilo la mitindo limeijumuisha mikoa mbalimbali ya Tanzania ikiwemo Mwanza,Dodoma,Arusha,Dar es Salaam.

Wednesday, November 6, 2013

MISS UNIVERSE TANZANIA ATAMBA MOSCOW

 
MISS Universe Tanzania, Betty Boniface Omara ametamba katika maonyesho ya mavazi kwa warembo 85 wanaowania taji la Miss Universe la mwaka huu mjini Moscow.

Katika mashindano hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Vegas Mall, vazi la Betty lililobuniwa na mbunifu anayekuja kwa kasi nchini, Mwanakombo Salim, lilipendwa na mashabiki wengi na anamatarajio makubwa kushinda taji hilo wakati wa fainali za mwaka huu zilizopangwa kufanyika Jumamosi.

Vazi hilo limechorwa na wasanii wa Tingatinga, Said Kambili na Mimus, michoro ambayo ni maarufu nchini iliyoasisiwa na msanii maarufu wa zamani, hayati Edward Tingatinga. Vazi hilo hilo mbali ya kudumisha utamaduni wa Tanzania, pia limechorwa michoro mbali mbali ya kuvitangaza vivutio vya kitalii.

Vazi hilo pia lina nakshi za mkeka na miba ya  mnyama maarufu ajulikanaye kwa jina la Nungunungu. Vilevile pia umetumika kama njia ya kumuonyesha ndege Tausi kama inavyoonekana rangi za mkeka kwenye mkia na kilemba kichwani mwake.

Lengo kuu la nguo na michoro hii ni kutangaza kazi za mikono na  utalii wa Tanzania na miongoni mwa michoro iliyoonyeshwa ni Duma, Tembo na Twiga vilevile imeonyesha ndege na mali asili zipatikanazo Tanzania kama vile Tausi, vipepeo, mimea na Mlima Kilimanjaro.

Mashindano ya Miss Universe Tanzania 2013 yamedhaminiwa na hifadhi ya Taifa Tanapa.