Wednesday, September 25, 2013

HAFSA KAZINJA AMUENZI MZEE MUHIDINI GURUMO.

MALKIA wa Zouk Tanzania Hafsa Kazinja aachia nyimbo ijulikanayo kama  “NIMUOKOE NANI” ikiwa ni moja ya njia ya kumuenzi Mzee Muhidin Maalim Gurumo ambaye amestaafu rasmi fani ya muziki baada ya kufanya kazi hiyo akiwa na bendi mbalimbali tokea mwaka wa 1960.

Kazinja  ambaye ameibuka upya baada ya kimya cha muda mrefu katika fani hiyo  akiwa na ingizo lake la kwanza kati  ya kumi alizoziandaa kwa kuimba wimbo maarufu wa NUTA Jazz Band uitwao “NIMUOKOE NANI” ambao anauouleta hewani katika mahadhi ya Zouk.

“Nimeamua kuimba wimbo huu wa “NIMUOKOE NANI” ili  kumuenzi gwiji huyu wa muziki kwani wakati yeye anastaafu na mimi ndiyo naibuka upya baada ya kukaa kimya kwa muda”, anasema Hafsa ambaye alitoka kwa wimbo wake wa “PRESHA” aliomshirikisha Banana Zorro.

Hafsa alisema  ukimya wake umetokana na kufanya utafiti na kujifunza kwa undani zaidi fani ya muziki na akipata mawaidha kutoka kwa wanamuziki nguli ndani nan je ya nchi wakiwemo Muhidin Maalim Gurumo, Omar Mkali, Abdul Salvador na Lokassa ya Mbongo wa Congo aliyekutana na kufanya naye kazi alipokuwa ziarani Marekani hivi karibuni

Kazinja alisema ataitambulisha rasmi ngoma ya “NIMUOKOE NANI” katika tamasha la kumuenzi Mzee Gurumo lililopangwa kufanyika OKtoba 1, 2013 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.

“Natumaini wapenzi wa muziki watafurika kwa wingi kwenye tamasha hilo nami naahidi kuitendea haki ngoma ya “NIMUOKOE NANI” hivyo wasikose kuja kujionea wenyewe jinsi sie wa kizazi kipya tunavyoweza kufanya kazi na wakubwa wetu wa kazi, anaongezea Hafsa ambaye pia anaandaa video yake pamoja na ya ngoma zake zingine mpya"alisema.

Kazinja alisema nyimbo hiyo “NIMUOKOE NANI” ameiandaa katika studio za OM Productions ya jijini Dar es salaam chini ya wanamuziki nguli, Abdul Salvador na Omari Mkali.

Pia Kazinja alisema alifurahishwa baada ya kupata baraka zote za kuuimba nyimbo hiyo kutoka kwa mtunzi na mwimbaji wake Mzee Gurumo mwenyewe.

No comments:

Post a Comment